HOTELI ya kimataifa ya Serena jana ilikumbwa na msukosuko wa
kuandamwa na waandishi wa habari baada ya kusambaa kwa tetesi kuwa imefungwa
kwa amri ya serikali kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.
Tetesi hizo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana
asubuhi, zikieleza kuwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wameifunga hoteli
kufunga kwa kukwepa kuliko kodi serikalini.
Mbali ya kusambazwa kwa uvumi huo, zilitumwa pia picha
zilizokuwa zikionyesha sehemu ya hoteli hiyo ikiwa imezungushwa uzio uliokuwa
na rangi nyeupe na nyekundu ambao ni alama inayotumika kuonyesha kusitisha kwa
huduma katika eneo hilo.
Tetesi hizo zilikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa uongozi wa
hoteli hiyo ulikuwa mbioni kubadilisha jina kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.
Hata hivyo, mwandishi wetu baada ya kufika hotelini hapo kwa
lengo la kufuatilia ukweli wa tetesi hizo alikuta shughuli za ukarabati wa
sehemu ya kupokea wageni zikiendelea, huku wageni wakielekezwa kutumia mlango
wa dharura ambako kumetengezwa sehemu ya muda ya kupokelea wageni.
Uongozi wa Hoteli ya Serena kupitia Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko,
Seraphine Lusala, ulilazimika kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ukikanusha
kufungwa kwa hoteli hiyo na kusisitiza kuwa kinachoendelea hotelini hapo ni
matengenezo.
“Si kweli kama hoteli imefungwa, tunafanya matengenezo na
yalikuwa yafanyike tangu miaka mitatu iliyopita, kilichofanyika sasa ni
kubadilisha eneo la mapokezi yaliyohamishiwa milango mingine na tumeanza na
eneo hilo pamoja na sehemu ya mazoezi,” alisema Lusala.
Alisema matengenezo hayo yanalenga kuifanya hoteli hiyo kuwa ya
kiwango cha juu zaidi na yatachukua miezi 10.
Lusala alisema awamu ya kwanza ya matengenezo itachukua miezi
minne na miezi minne ijayo itahusu matengenezo sehemu ya vinywaji, chakula,
eneo la uwanja na baadaye maeneo mengine ya wazi.
